Skip to main content

TAMKO LA KIKOSI KAZI CHA KUPINGA ADHABU YA VIBOKO SHULENI KUHUSU TAARIFA ZA KIFO CHA MWANAFUNZI BUNDA

31 Aug 2026 Tanzania

Kikosi Kazi cha Kupinga Adhabu ya Viboko Shuleni Tanzania kimeeleza masikitiko na wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za kifo cha mwanafunzi Petro Chisumo (23) wa Shule ya Sekondari Makongoro, Bunda, Mara, baada ya kudaiwa kupewa adhabu ya viboko shuleni. Kikosi Kazi kinatoa pole kwa familia na jamii ya Bunda na kutoa wito kwa mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina, huru, wa haraka na wa uwazi kuhusu tukio hilo, huku kikisisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa nidhamu shuleni na matumizi ya njia chanya na zisizo za ukatili katika kuwalea na kuwaelimisha watoto.

Bunda, Mara – 28 Agosti 2026.

 

Kikosi Kazi cha Kupinga Adhabu ya Viboko Shuleni kimepokea kwa masikitiko na wasiwasi mkubwa taarifa zinazosambaa kuhusu kifo cha mwanafunzi Petro Chisumo (23), aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Makongoro, Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Tanzania, Mkoa wa Mara iliyochapishwa na vyombo vya habari, imeeleza mnamo Agosti 19, 2026 mwanafunzi huyo Pamoja na wenzake wakiwa shuleni, walidaiwa kupewa adhabu ya viboko kutoka kwa walimu wao kwa sababu ya ufaulu wa chini katika mitihani, iliyopelekeakupata matatizo ya kiafya na baadaye kufariki akiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Aidha, taarifa hizo zinaeleza kuwa Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio hilo na linawashikilia walimu 6.

 

Kikosi Kazi kinatoa pole za dhati kwa familia, ndugu, jamaa, wanafunzi, walimu na jamii ya Bunda kufuatia msiba huu. Tunatambua kuwa kifo cha mtoto ni pigo kubwa kwa familia na jamii nzima, na tunasisitiza umuhimu wa kupata ukweli kamili kuhusu mazingira yaliyopelekea kifo cha mwanafunzi huyo.

 

Msimamo wa Kikosi Kazi.

 

Kikosi Kazi kinasisitiza kwamba shule inapaswa kuwa sehemu salama kwa kila mtoto kujifunza, kukua na kutimiza ndoto zake, bila kuhofu kupata madhara ya kimwili au kisaikolojia kutokana na hatua za kinidhamu.

 

Tunatambua kuwa Tanzania ina mfumo wa kisheria unaodhibiti matumizi ya adhabu ya viboko shuleni. Education (Corporal Punishment) Regulations, 2002 zinaweka masharti kuhusu mazingira ambayo adhabu hiyo inaweza kutolewa na zinataka iwe ya kiasi, ikizingatia uzito wa kosa, umri, jinsia na afya ya mwanafunzi, na kutokuzidi viboko vinne kwa tukio moja.

 

Aidha, Sheria ya Mtoto (Law of the Child Act, 2009 [R.E. 2023]) inamtaka kila mtoto kulindwa dhidi ya mateso, adhabu ya kikatili, isiyo ya kibinadamu au inayodhalilisha, pamoja na aina yoyote ya marekebisho ya tabia ambayo si ya kiasi na inayoweza kumletea mtoto madhara.

 

Kwa msingi huo, Kikosi Kazi:

 

  1. Kinatoa wito kwa Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine husika kufanya uchunguzi wa kina, huru, wa haraka na wa uwazi ili kubaini mazingira yote ya tukio hili, ikiwa ni pamoja na aina ya adhabu iliyotolewa, namna ilivyotekelezwa, hatua zilizochukuliwa baada ya mwanafunzi kupata matatizo na chanzo halisi cha kifo chake.

  2. Kinatoa wito kwa mamlaka za elimu kuhakikisha kuwa hakuna hatua yoyote ya kinidhamu shuleni inayokiuka sheria, taratibu na haki za mtoto, na kwamba walimu na viongozi wa shule wanawajibishwa pale ambapo kuna ukiukwaji wa sheria au taratibu.

  3. Kinatoa wito kwa mamlaka za elimu kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa adhabu za kinidhamu shuleni, ili kuhakikisha kwamba taratibu zilizowekwa zinatekelezwa kwa usahihi na kwamba afya na usalama wa mtoto vinapewa kipaumbele.

  4. Kinahimiza shule kuongeza matumizi ya njia chanya na zisizo za ukatili katika kujenga nidhamu, ikiwa ni pamoja na nidhamu chanya (positive discipline), ushauri nasaha, mwongozo na mbinu nyingine zinazomsaidia mtoto kuelewa na kurekebisha tabia bila kumweka katika mazingira ya madhara.

  5. Kinatoa wito kwa walimu, wazazi, wanafunzi na jamii kwa ujumla kuendelea kutoa taarifa za vitendo vyovyote vya ukatili au matumizi mabaya ya adhabu shuleni kupitia mamlaka zinazohusika, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

  6. Kinatoa wito kwa Serikali kuendelea kupitia na kuimarisha mfumo wa kisheria na kisera unaosimamia nidhamu shuleni, kwa kuzingatia wajibu wa Tanzania wa kulinda haki, utu, usalama na ustawi wa kila mtoto.

 

Wito kwa jamii

 

Kikosi Kazi kinawakumbusha wadau wote kwamba nidhamu na ulinzi wa mtoto si vitu vinavyopingana. Mtoto anaweza kufundishwa uwajibikaji na kuheshimu kanuni bila kutumia njia zinazoweza kumuumiza, kumdhalilisha au kuhatarisha maisha yake.

 

Tukio hili linapaswa kuwa wito wa pamoja wa kujiuliza kwa kina kuhusu namna tunavyotekeleza nidhamu katika shule zetu na kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anayepoteza maisha, kupata ulemavu au kupata madhara ya kudumu kutokana na hatua iliyokusudiwa kumrekebisha kitabia.

 

Kikosi Kazi kitaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa rasmi kuhusu tukio hili na kinatarajia mamlaka husika kutoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi kwa uwazi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

 

Mtoto anahitaji nidhamu, lakini nidhamu isiyomdhuru.

Shule salama ni shule isiyo na ukatili.

 

Imetolewa na:Kikosi Kazi cha Kupinga Adhabu ya Viboko Shuleni Tanzania

Save the Children/Tanzania (SCT), Women in Law and Development in Africa (WiLDAF), UNICEF, World Health Organization (WHO), HakiElimu, Zanzibar Children Right Forum (ZCRF), Zanzibar Female Lawyers Association (ZAFELA), Shule Direct, Children’s Dignity Forum (CDF), Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Msichana Initiative, Legal and Human Rights Centre (LHRC), FAWE Tanzania, ZAPHA+, Zanzibar Legal Aid and Human Rights Organization, Tanzania Media Women Association (TAMWA), Zanzibar Female Lawyers Association, (ZAFELA), Christian Social Services Commission (CSSC)
 

Related News